Je, unaujua Faida za ViCoBa kwa wananchi wa hali ya chini

Vicoba (Village Community Bank) ni mfumo wa kuweka na kukopa kwa wanachama waliojiunga kwa pamoja na kuunda kikundi kwa malengo ya kujikwamua kutoka kwenye umaskini.

Mfumo huu ulianza Tanzania miaka 10 iliyopita na umeonyesha mafanikio makubwa kwa wanachama kukopeshana na kusaidiana katika matatizo mbalimbali na pia kuanzisha miradi ya kiuchumi.

Vicoba vimesaidia asilimia kubwa ya wananchi kujikwamua na umaskini ambao umetawala. Kupitia Vicoba, jamii imepanua maendeleo yake na taifa kwa ujumla.

Vicoba hutoa mafunzo ya kuongeza ujuzi wa biashara kwa wanachama kupewa fursa au kipaumbele cha kupata mafunzo na ujuzi wa biashara ili kuleta ongezeko na faida kwenye biashara wanazojihusisha nazo.

Hutoa mafunzo juu ya ujasiriamali na biashara mbalimbali. Hufundisha jinsi ya kuwa mjasiliamali na kubainisha anatakiwa aweje, nini maana yake na faida zake.

Mara nyingi huwafundisha kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwamo sabuni za maji, magadi na bidhaa nyinginezo.

Huwasaidia wanachama kutafuta masoko ya uhakika kwa ajili ya kusambaza na kuuza bidhaa zao kwa bei yenye faida bila wao kunyonywa.

mfano wa kadi ya hisa za VICOBA

Wanachama wanaweza kupata mitaji ya biashara kutoka kwenye kikundi ambayo itawawezesha kuanzisha au kuendeleza biashara zao. Biashara za wanachama zitaweza kukua kutoka kwenye kiwango cha chini au kutoka kwenye biashara ya mtaji mdogo mpaka kuwa mkubwa.

Ndiyo kusema si ajabu mjasiriamali aliyeanzia kwenye Vicoba akajikuta anakuwa mfanyabiashara mkubwa anayetegemewa na Taifa katika kuongeza mapato yake kupitia kodi mbalimbali.

Unaweza usiamini lakini haya yanawezekana iwapo mhusika atakuwa makini na kufuata kanuni sahihi za kibiashara zilizobuniwa vizuri.

Vicoba pia husaidia kukuza uchumi wa wanachama au wanakikundi kutokana na shughuli ambazo wamekuwa wakijihusisha nazo na ambazo zimekuwa zikiwaletea maendeleo.

Familia ambazo zimekuwa zikijihusisha na vikundi hivi, zimeukuza uchumi na kupiga hatua nzuri ya kujikimu.

Kukua huku kwa uchumi wao kumeziondolea familia mizigo mingi ambayo ilikuwa ikiwakabili ikiwamo ile ya, kusomesha watoto pamoja na pesa ya matibabu pale kunapokuwa na mtu mgonjwa katika familia.

Hutoa mikopo kwa wanachama, ambayo inawasaidia wanachama (jamii) katika shughuli za kimaendeleo ikiwamo biashara.

Lakini mikopo hii ni nafuu kwa sababu inakuwa na riba ndogo kuliko mikopo ya taasisi nyingine. Riba yake haizidi asilimia 10 katika marejesho yake, hii inasaidia wanachama waweze kurejesha kwa wakati na kwa wepesi.

Wanachama wa Vicoba wana umoja ambao pindi panapotokea matatizo ikiwamo misiba na ugonjwa, husaidiana.

Endapo mwanachama mmoja au zaidi wamefikwa na msiba, kuugua au kuuguliwa, wanachama husaidiana kwa asilimia kubwa kwenye shughuli hiyo kama vile inavyokuwa kwa ndugu wa familia moja.

Pia, Vicoba vinaleta umoja na ushirikiano katika jamii. Wanachama hufanya kazi au vitu vya maendeleo kwa umoja na kwa kushirikiana wote kuanzia kwa viongozi na watu wote.

Vinadumisha upendo baina ya watu kutokana kuwa bega kwa bega katika matatizo na katika sherehe na shughuli mbalimbali.

Kutokana na utaratibu wa wanakikundi kushirikiana katika misiba, maradhi na sherehe, kitendo hicho kinawafanya kuwa karibu na kutambuana.

Pia vikundi hivi vinatoa ajira kwa wanachama. Vimekuwa vikitoa ajira kwa wanachama kutokana na miradi mbalimbali ambayo wamekuwa wakianzisha kutokana na mafunzo ya biashara wanayopata.

Wanachama wametumia fursa hizo kama moja wapo ya sehemu ya kupata ajira na kujikwamua kiuchumi. Hii siyo kwa wasio na ajira tu, bali hata wale walioajiriwa, lakini kipato chao ni kidogo.

Forum Moderator

About The Author

Leave A Comment?

You must be logged in to post a comment.