Forum Navigation
You need to log in to create posts and topics.

JINSI MFUMO WA VICOBA UNAVYOFANYA KAZI TANZANIA

VICOBA (Village Community Bank) ni mfumo wa kuweka na kukopa kwa wanachama waliojiunga kwa pamoja na kuunda kikundi kwa malengo ya kujikwamua kiuchumi. Mfumo huu ulianza Tanzania miaka kumi iliyopita na umeonyesha mafanikio makubwa kwa wanachama wake kuweza kukopeshana, kusaidiana katika matatizo mbalimbali, kuanzisha miradi ya pamoja ya kiuchumi.

LENGO/MADHUMUNI YA KUUNDA VICOBA
Madhumuni ya kuunda vicoba ni kuunganisha nguvu na rasilimali za wanachama ili kuondoa umaskini na kuleta maendeleo kwa kufanya yafuatayo:-

  • Kuchangia/kununua hisa
  • Kuchangia mfuko wa jamii
  • Kuendesha mfuko wa kuweka na kukopa
  • Kushiriki katika mafunzo ya kuongeza ujuzi wa biashara, uongozi na uanzishaji wa shughuli mbalimbali za pamoja za maendeleo.
  • Kutafuata soko la pamoja na la uhakika kwa bidhaa za wanakikundi 

Kuna tofauti gani kati ya VICOBA na SACCOS?
VICOBA na SACCOS ni vikundi vya kiuchumi vyote vina malengo sawa isipokuwa mfumo wa uendeshaji.

  1. Katika VICOBA wanachama uweka kiwango cha hisa na mara nyingi huanzia Sh.1000 na kuendelea, kiwango hicho ni kidogo ukilinganisha na kiwango cha hisa katika SACCOS.
  2. WanaVICOBA umaliza mzunguko wao baada ya miezi kumi na mbili (12) na kufanya tathmini ikiwemo kugawana makusanyo na faida.
  3. Riba ya mkopo katika VICOBA ni ndogo (mara nyingi haizidi 10%)
  4. Kikundi cha VICOBA kinaundwa na wanachama 15-30, wanaoishi eneo moja au wanaofanya kazi pamoja.
  5. Gharama za uendeshaji wa VICOBA ni ndogo kwani hakuna ofisi (wanachama huchagua mahali pa kukutana kwa muda usiozidi saa moja), vile vile viongozi wa VICOBA hawaajiriwi (wanafanya kazi za kujitolea)Vicoba ikikuwa inaweza kuunda SACCOS. Mfumo wa Vicoba ni mzuri hasa kwa falsafa ya kuanza kidogo ili kuwa na kitu kikubwa hapo baadae. Licha ya kujihusisha na shughuri za kuweka na kukopa, wanavicoba husaidiana katika matatizo mbalimbali kama msiba na ugonjwa. Vile vile wanavicoba wanaweza kuanzisha mradi wa pamoja wa kikundi kwa kuunganisha rasirimali ndogo walizonazo. 

Hatua za Kuunda kikundi cha VICOBA

  1. Watu wenye wazo la kuanzisha kikundi kukutana (watu hao wasipungue kumi na tano na wasizidi therathini)
  2. Wanachama kukusanya fedha za kiingilio (mara nyingi ni Sh. 10,000) kwa mwanachama. Fedha hiyo hutumika kununua vifaa kama leja,kasiki n.k. Fedha ya kiingilio vilevile hutumika kugharamia mafunzo ya awali na gharama ya usajiri wa kikundi)
  3. Wanachama kuanza mafunzo yatakayosimamiwa na mwalimu mtaalamu wa mfumo huu wa vicoba.
  4. Wanachama kutunga katiba na sheria zitakayojumuisha kiwango cha hisa, mfuko wa jamii, siku ya kukutana n.k

WADAU WANAOTEKELEZA MFUMO VICOBA TANZANIA

Kwa miaka mingi sasa wadau mbalimbali wanahamashisha vikundi katika maeneombalimbali na miongoni mwa wadau hao ni pamoja na IRCPT, UPEO, TEC, CCT, BAKWATA, AEE, Pathfinder International, AFRICARE, LAMP, LIWODET, MEPP, RUMAKI, Social EconomicDevelopment Initiative of Tanzania, SELL, VDSA, WWF, ORGUT, FLORESTA, ELCT(ND, ECD,Mbulu) TCRS, TANARELA, AXIOUS Foundation, WCST, ITECCO, Frankfurt Zoological Society, UYACODE, YWCA, EFG na wengine wengi. Maeneo mbalimbali ya Tanzaniayameweza kufikiwa japo siyo wadau wote wanatekeleza mfumo huu kama inavyotakiwa.

UMADHUBUTI WA VICOBA

  1. Uanzishaji wa kikundi cha VICOBA hauhitaji mtaji. Makusanyo ya kila wiki yanayotolewa na wanakikundi ndiyo huanzisha mfuko wa kukopesha.
  2. Vikundi huanzishwa karibu na maeneo ya wanachama wanayoishi hivyo hupunguza gharama ya nauli na matumizi mabaya ya muda.
  3. Mikopo ya VICOBA haina ukiritimba kama fedha zipo, maana             wanakikundi          wanajua mwenendo mzima wa fedha za kikundi kwa sababu shughuli    zote za  kikikundi hufanywa mbele ya wanakikundi wote.
  4. Kupitia mfumo huu wanakikundi wanatumia mikutano ya kikundi kama     sehemu ya kujifunza mambo mengine kama vile elimu ya biashara, masuala ya kisheria,  ukatili wa kijinsia, jinsi ya kuhudumia watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi,          kuelimishana haki za kila mtu na mambo mengine ambayo wanakikundi          wanaona ni muhimu kwao kuyajadili na kujifunza.
  5. Mfumo wa utunzaji wa kumbukumbu ni rahisi ambao unawawezesha wanakikundi kusimamia kumbukumbu zao za fedha bila kuhitaji elimu ya juu ya utunzaji wa fedha.
  6. Ziada ya mikopo inayopatikana hutolewa mgao kwa wanakikundi wote mwisho kutokana na  idadi ya hisa zake.

Imeandikwa na Ombeni Haule

Kwa elimu na ushauri wasiliana nasi kwa simu namba 0659144660/0758069046